Jumatatu 28 Julai 2025 - 07:21
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan: Ubinadamu Unakata Roho Ghaza na Dunia Inatazama

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, katika tamko lake huku akionyesha wasiwasi mkubwa kuhusiana na janga la kibinadamu huko Ghaza, amelaani vikali ukimya mzito wa jumuiya ya kimataifa na ameitaka Pakistan ichukue jukumu la dhati na lenye athari zaidi kwenye kuwatetea wananchi wanyonge wa Palestina.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, katika tamko lake huku akionyesha wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ya kusikitisha katika Ukanda wa Ghaza, amesisitiza kuwa: Leo hii Ghaza, ubinadamu unakata pumzi za mwisho na janga kubwa linaendelea kutokea. Hali hii ya maumivu ni kofi kali usoni mwa dunia inayodai ustaarabu na haki za binadamu.

Ameongeza kuwa: Leo Ghaza imekuwa makaburi ya watu hai, si tu kwamba janga la kibinadamu limetokea, bali taasisi za kimataifa na mashirika ya haki za binadamu mbele ya jinai hizi za wazi ni watazamaji tu, na sauti ya watu wanyonge imepotea katika kelele za maslahi ya nguvu kubwa.

Mwanachuoni huyu mashuhuri wa Kipakistani ameendelea kukumbusha kuwa: Katika hali kama hii, tamko la hivi karibuni la Rais wa Ufaransa, licha ya kuwa na baadhi ya hoja zinazoweza kujadiliwa, ni hatua yenye kuleta matumaini katika kufichua ukweli wa dhulma dhidi ya watu wa Palestina, hii ni katika hali ambapo mwitikio wa Marekani, kama ilivyo daima, umejaa hila, kejeli na kuunga mkono waziwazi utawala wa Kizayuni, na unaonyesha kuwa nyuma ya pazia la dhulma hii isiyo na huruma, zipo sera zilezile za ujanja za Marekani.

Akiashiria nafasi ya kificho ya Magharibi na hasa Marekani, amesema kuwa: Marekani siyo tu kwamba haijafumba uso mbele ya jinai za Israel, bali kwa kuunga mkono kikamilifu utawala huo, inashiriki moja kwa moja katika kuendeleza dhulma na mauaji ya kizazi huko Ghaza. Mwitikio wao kwa maneno ya Rais wa Ufaransa pia ni jitihada ya kupotosha fikra za umma kuhusu ukweli mchungu wa Palestina.

Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, akihitimisha, amebainisha kuwa: Katika hali kama hii, wajibu wa Pakistan kama nchi ya Kiislamu, yenye demokrasia na nafasi muhimu katika eneo, ni mzito zaidi kuliko wakati wowote, sasa umefika wakati ambapo Pakistan isiwe tu sauti ya wanyonge, bali kwa kutumia uwezo wake wa kidiplomasia, kisiasa na kibinadamu, ijitahidi kwa dhati kusitisha jinai hizi, vilevile, ni lazima ifikishe ujumbe wazi wa taifa la Pakistan, ambalo limeghadhabishwa na maafa haya, kwa nguvu za dunia hasa Marekani; kwani kupuuza hisia hizi za wananchi kunaweza kuwa na athari pana na kubwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha